Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Ayatollah Musawi katika hotuba ya Sala ya Ijumaa mjini Baghdad alisema: “Kile tunachokiona leo ni matokeo ya miaka miwili ya mapambano na kujitolea kwa watu wa Gaza dhidi ya ujeuri wa Israel. Katika kipindi hicho, zaidi ya watu 260,000 wameuawa, kujeruhiwa au kupata ulemavu.”
Aliongeza kuwa: “Kuwepo kwa usitishaji mapigano hakumaanishi kufungwa kwa jalada la uhalifu dhidi ya raia, bali ni ukumbusho wa ulazima wa kuwafikisha wahalifu hawa kwenye vyombo vya sheria na kuadhibiwa.”
Imamu huyo wa Ijumaa alimshutumu vikali Trump kwa madai yake kwamba ndiye aliesababisha vita kusimama, akisema:
“Yule aliyeilisha mashine ya mauaji ya Kizayuni kwa silaha, msaada wa kisiasa na kinga ya vyombo vya habari, hawezi kamwe kuitwa mtu wa amani.”
Akaongeza kuwa: “Marekani ni mama wa uovu katika eneo hili, na ndiyo iliyompa Netanyahu ruhusa ya kufanya mauaji haya.”
Ayatollah Musawi pia alikemea vikali baadhi ya nchi za Kiarabu na Uturuki akisema:
“Ziliingia kwenye mazungumzo pamoja na Marekani na Israel, lakini hazikuweza hata kidogo kusimamisha mashambulizi. Kimya chao, kwa hofu ya kulinda tawala zao, kimekuwa ushirikiano wa moja kwa moja na wavamizi.”
Akiashiria mabadiliko ya msimamo wa baadhi ya nchi za Ghuba, alisema:
“Baada ya kutambua kuwa Marekani si tena mshirika wa kuaminika, zimeanza kuelekea ushirikiano na Urusi, China na Iran. Mazungumzo ya Ghuba–Urusi sasa yanaashiria uwezekano wa mabadiliko ya mizani ya nguvu katika eneo.”
Akaongeza kuwa: “Mwelekeo huu mpya unaonyesha kufahamu kwa kuchelewa kwamba enzi ya utegemezi kamili kwa Washington imekwisha.”
Kuhusu masharti ya usitishaji mapigano, Ayatollah Musawi alisema:
“Makubaliano hayo yanahusisha kuondoka kwa kiasi kwa wanajeshi wa Israel na kuachiliwa kwa baadhi ya wafungwa wa Kipalestina,”
lakini alionya kuwa Netanyahu hawezi kuaminika, kwani “uwezekano wa kuanza tena uvamizi upo wakati wowote.”
Alisisitiza: “Kusambaratishwa kwa harakati ya Hamas hakumo kwenye makubaliano haya, na Muqawama bado upo thabiti ukiwa na nguvu na silaha zake.”
Akaeleza kuwa kipimo cha ushindi si idadi ya mashahidi, bali kutimia kwa malengo ya kimkakati.
“Hivyo basi, Muqawama umeshinda kwa kuweka masharti yake na kuvuruga njama za adui za kuuangamiza.”
Ayatollah Musawi aliwasifu viongozi wa Muqawama akisema:
“Wamejitolea nafsi zao kwa ajili ya uhuru wa taifa lao, huku Israel, licha ya propaganda zake, ikipata kushindwa kimaadili na kimkakati.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alionya kuhusu mpango wa ‘Mashariki ya Kati Mpya’ — mradi unaolenga kugawa nchi za Kiarabu na kuongeza ushawishi wa Israel katika eneo.
Akasema: “Marekani bado inaendelea kutumia Israel kuchochea vita na machafuko.”
Kwa mujibu wake, “njia pekee ya kukabiliana na mpango huo ni umoja na nguvu ya pamoja ya mataifa ya eneo hili.”
Mwisho wa hotuba yake, Ayatollah Musawi aliwataka nchi za Kiislamu na Kiarabu kuimarisha ushirikiano na kujenga nguvu huru zisizo tegemea Marekani, akisema:
“Kama Waislamu na Waarabu tungelikuwa wamoja, wala Trump wala yeyote mwingine asingethubutu kutulazimisha masharti yake, na Israel isingemwaga damu hata ya mtoto mmoja huko Gaza.”
Pia aliwakumbusha wananchi wa Iraq wawe macho kuelekea uchaguzi ujao, akisema:
“Uchaguzi huo unaweza kuamua hatma ya Iraq — aidha katika utulivu au machafuko.”
Your Comment